UNESCO: Urithi wa Kiafrika bado haujatambuliwa kulingana na umuhimu wake wa kihistoria | | Habari za UN
Ikiwa leo ni siku ya urithi wa dunia wa Afrika, shirika la elimu, sayansi na utamaduni la Umoja wa Mataifa UNESCO linasema urithi huo ambao thamani yake ya kipekee inaadhimisha leo, bado haujatambuliwa kulingana na umuhimu wake wa kihistoria, wa kibinadamu na wa asili.
Taarifa ya Evarist Mapesa inafafanua zaidi.
Kupitia ujumbe wake wa siku hii mkurugenzi mkuu wa UNESCO Audrey Azoulay amesema baada ya kupitishwa mkataba wa urithi wa dunia miaka 50 iliyopita na kuanza kutekelezwa rasmi mwaka 1978, miongoni mwa maeneo 12 ya kwanza kuingizwa kwenye orodha ya urithi wa duniani matatu yalikuwa barani Afrika - hii ikimaanisha kwamba robo ya maeneo ya awali yaliyochaguliwa yalikuwa barani humo.
Hata hivyo amesema “Leo, hii, Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara inachukua takriban moja ya kumi ya maeneo yote yaliyoorodheshwa ingawa thamani ya urithi wake wa kipekee, bado haijatambuliwa. Ili kukabiliana na hali hii, na kuupa heshima ipasavyo kutokana na fikra za binadamu na kazi za asili zinazopatikana barani Afrika, UNESCO imeliweka bara hili kuwa kitovu cha mkakati wake wa urithi wa dunia.”
Mkuu huyo wa UNESCO amesisitiza kuwa kuna haja ya kufikiria upya utekelezaji wa mkataba wa urithi wa dunia ili kukabiliana na changamoto zitakazoukabili miaka mingine 50 ijayo na hatimaye kufanikisha msingi wa mkataba huo wa urithi wa kipekee wa dunia nzima.
Ameongeza kuwa “Ni kwa sababu ya upekee wake wa kina, utofauti wake na utajiri wake ndiyo maana urithi wa Kiafrika ni wa ulimwengu wote na unahitaji tuutilie maanani. Mifano ya urithi huu ni pamoja na misikiti minane ya mtindo wa Wasudan nchini Côte d'Ivoire ambayo iliingizwa kwenye orodha ya urithi wa dunia mwaka jana, mbuga ya taifa ya wanyama ya Ivindo Gabon ambayo inahifadhi wanyama wengi walio hatarini kutoweka ikiwemo tembo.”
Azoulay amehitimisha ujumbe wake kwa ahadi kwamba “Ili kutambua vyema urithi huu wa Kiafrika na kuwezesha mchango wake kwa urithi wetu wa dunia, tutahakikisha kwamba kufikia mwaka wa 2025, mataifa yote ya Afrika yanayotaka kufanya hivyo yatakuwa yamewasilisha angalau ombi moja la kujumuishwa kwenye orodha ya urithi wa dunia kwa msaada wa kisayansi na kiufundi kutoka kwa Shirika la UNESCO.”
Shirika hilo linasema “ingawa Afrika ina uwakilishi mdogo kwenye orodha ya urithi wa dunia, mali za Kiafrika zinachukua takribani asilimia 12 ya maeneo yote yaliyoorodheshwa duniani, na asilimia 39 ya mali hizi ziko kwenye orodha ya urithi wa dunia ulio hatarini.”
Ukikabiliwa na vitisho mbalimbali vya kisiasa, mabadiliko ya tabianchi, maendeleo yasiyodhibitiwa, ujangili, machafuko ya kiraia na ukosefu wa utulivu, maajabu mengi ya urithi wa Afrika yana hatari ya kupoteza thamani yake bora ya ulimwengu.
“Kwa hiyo ni suala la dharura zaidi kuliko wakati mwingine wowote kwamba urithi huu usiweze kubadilishwa ulindwe na kuhifadhiwa kwa ajili ya kufurahiwa na vizazi vijavyo.”
Siku hii huadhimishwa kila mwaka Mei 5 na UNESCO inasema ni fursa kwa watu wote duniani, na hasa Waafrika, kusherehekea urithi wa kipekee wa kitamaduni na wa asili wa bara hilo.