Huduma za fedha mtandao zamwondolea mwanafunzi adha ya kufuata fedha benki | | Habari za UN
Misri, taifa lenye watu milioni 100 hivi sasa, lakini ni asilimia 30 tu ya watu hao yaani watu milioni 36.8 ndio wenye akaunti za benki. Katika zama hizo za huduma za fedha kimtandao, mashirika ya mawasiliano ya simu yanaingia ubia na benki ili kupanua wigo wa huduma hizo. Ukosefu wa huduma za fedha kimtandao zinakuwa kikwazo kwani wananchi hupoteza muda mwingi benki kusubiria malipo ambayo wangaliweza kuyapokea kupitia simu za kiganjani au rununu. Shuhuda pande zote mbili hizo ni msichana mmoja mkazi wa Cairo nchini Misri kama anavyosimulia Assumpta Massoi kwenye makala hii iliyoandaliwa na shirika la Umoja wa Mataifa la Mawasiliano duniani, ITU.
Kukurukakara za Cairo, mji mkuu wa Misri huu. Bajaji huku, magari kule, watu huku na kule. Alimradi harakati za asubuhi kwenye mitaa ya mji huu. Na miongoni mwa watu hao ni Gehad, mwanafunzi huyu wa kike. Lakini asubuhi hii, haendi shuleni, bali anaenda benki. Kulikoni, Gehad anasema, wazazi wangu walipeana talaka kama miaka kumi na mitano iliyopita. Malipo ya masurufu, kutoka kwa baba kwenda kwa mama, tulianza kupokea miaka mitano iliyopita kupitia benki ya Nasser. Waliweza kupokea fedha hizo, baada ya usaidizi kutoka wizara ya mshikamano wa kijamii ya Misri.
Hata hivyo kulikuwa na changamoto. Anasema, "Nilidamka kuwahi benki. Na nilisimama kwenye mstari mrefu sana. Kwa hiyo, siku ya kwenda benki, ilikuwa ni siku ngumu sana kwangu." Na hakika katika video hii ya shirika la Umoja wa Mataifa la Mawasiliano Duniani ITU, msururu ni mrefu katika benki ya Nasser. Wake kwa waume, hali kadhalika vijana wa kiume na wa kike akiwemo Gehad. Na pahala pa kuketi, viti ni vichache. Kwa ufupi, msongamano ni mkubwa. Serikali ya Misri kwa ushirikiano na benki ya Nasser wakabaini tatizo na hivyo wakaibuka na jawabu. Kama anavyosema, Ahmed Kedir, afisa mwandamizi kutoka kampuni ya mawasiliano ya simu Orange. "Wizara ya mshikamano wa kijamii na benki ya Nasser waliingia ubia na kampuni Orange. Ubia huu, umeundwa kuwawezesha wateja wa benki ya Nasser kupokea malipo yao ya masurufu kila mwezi wakiwa nyumbani. Na watapokea ujumbe mfupi kupitia simu yao kwamba wamepokea malipo yao na hivyo, anaweza kumtumia mtu yeyote fedha, au kulipa malipo yoyote, au kutoa fedha kupitia matawi ya Orange, mawakala, au kwenye mashine ya kutolea fedha."
Hii ilikuwa ni habari njema kwa Gihad. Akionekana kwenye video hiyo, akipokea ujumbe mfupi wa malipo, na kisha akiwa nyumbani, anasema, "Zamani nililazimika kukosa madarasa ya somo shuleni. Kwa sababu, nililazimika kuenda benki kuchukua fedha. Lakini sasa, naweza kupata wakati wowote ule." Harish Natarajan kutoka benki ya dunia, anaona hali ni mafanikio kubwa kwa wateja na watu wa huduma. "Huduma za fedha kimtandao zimeondoa kwa kiasi fulani, huduma za malipo kwa benki, kama huduma inayojitegemea. Ila sasa ni hatua moja mbele. Iwapo akaunti yako iko benki, bado unaweza kufanya miyamala na akaunti yako kupitia huduma zinazotolewa na mtoa huduma wa tatu."