COVID-19 ilidhihirisha kila mkazi wa dunia ana thamani yake - Susan Mang'eni | | Habari za UN
Jukwaa la Umoja wa Mataifa la ufadhili kwa ajili ya maendeleo 2023 FfD linaendelea kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa katika jaribio la kubadilisha mfumo wa fedha wa kimataifa na kurejesha ajenda ya maendeleo endelevu ya 2030 katika mstari unaotakiwa ikiwa imesalia chini ya miaka saba kufikia ukomo.
Nchi, hususan zinazoendelea zinahaha kuhakikisha zinatimiza malengo yake kwa kila hali na miongoni mwao ni Kenya ambapo Susan Auma Mang'eni Katibu Mkuu wa Idara ya Ukuzaji wa Biashara Ndogondogo iliyo ndani ya Wizara Mpya ya Ushirika na Ukuzaji wa Biashara Ndogondogo au Ujasiriamali nchini humo anahudhuria kongamano hilo na amemweleza Flora Nducha wa Idhaa hii ya Kiswahili amekuja na ujumbe maalum kutoka Kenya.
“Kwanza nimekuja hapa ili kuwasilisha ujumbe wetu wa Kenya hasa tunavyoona ufadhili wa maendeleo, kwa sababu lile janga la COVID-19 limedhihirisha bayana kwamba hakuna sehemu yoyote hapa duniani ambayo haina faida ya mambo ya uchumi, hakuna binadamu yeyote ambaye hana uzuri wake, hana thamani ya kiuchumi. Na limeonyesha ya kwamba wakati ule ambao tulikuwa katika zile hekaheka tukijaribu kujiuliza ni jinsi gani tutakabvyoliangamiza hili janga la COVID tulijiuliza maswali lakini hatukuwa na majibu , sasa ilibidi ya kwamba kila sehemu duniani kila nchi ianze kujifikiria kuona ya kwamba ni lipi sisi tunaweza fanya kuangamiza COVID-19. Na tunaona ya kwamba kuna nchi nyingi sana katikia hii dunia ambazo ziliweza kushinda haya madhara ya COVID -19 na sasa hivi imeonesha ya kwamba kama dunia sasa lazima tuanze kujiuliza ni jinsi gani sasa tutakavyoweza kukuza uchumi wetu, ili tuweze kuboresha Maisha ya wananchi wetu ili hapo baadaye litakapotokea tena janga kama hili tusife sana kama jinsi tulivyopoteza wananchi wetu.”
Akaenda mbali zaidi na kusema rasilimali watu ipo wanachohitaji sasa na wanachokiomba kwenye mkutano huu ni ufadhili ili kufikia malengo ya maendeleo na ukuzaji uchumi wao.
“Tunaweza kusema kwamba majibu mengi yako katika urithi wetu kama nchi na hasa sisi hapo Kenya tunatambua ya kwamba urithi wetu uko katika wananchi wetu, kwa watu wetu ambao wana bidii, wana ndoto nzuri na wameonesha kwamba wao wanaweza kufanya lolote ili kuendelea kimaisha. Na tumeona kwamba ukienda popote pale utaona rasilimali ipo, na hii rasilimali utaitambua kupitia utamaduni wetu, jinsi ambayo tunaishi na jinsi ambavyo tunashirikiana na wengine kwa vyakula vyetu, kwa kilimo chetu , kwa bidii yetu, ndio inaonesha kuwa hiyi ndio rasilimali yetu.”